Monday, May 14, 2012

KOCHA KIM AITA 25 TAIFA STARS

Kikosi cha Taifa Stars.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen leo (Mei 14 mwaka huu) ametangaza kikosi cha wachezaji 25 kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia hatua ya makundi Kanda ya Afrika dhidi ya Ivory Coast.
Akitangaza kikosi hicho ambacho kitaingia kambini kesho kutwa (Mei 16 mwaka huu, Kim amesema uteuzi wake umezingatia uwezo wa mchezaji uwanjani, nafasi anayocheza na ubora wake.
Wachezaji walioitwa ni makipa; Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ally (Azam) na Deogratius Munishi (Mtibwa Sugar). Mabeki ni Nassor Masoud Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Amir Maftah (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Simba), Waziri Salum (Azam), Shomari Kapombe (Simba) na Juma Nyoso (Simba).
Viungo ni Mwinyi Kazimoto (Simba), Salum Abubakar (Azam), Nurdin Bakari (Yanga), Jonas Mkude (Simba), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Edward Christopher (Simba- U20), Mrisho Ngasa (Azam) na Frank Domayo (JKT Ruvu- U20).
Washambuliaji ni Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo), Ramadhan Singano (Simba-U20), Simon Msuva (Moro United- U20), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo), Haruna Moshi (Simba) na John Bocco (Azam).
Stars inayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro itacheza mechi ya kirafiki nyumbani Mei 26 mwaka huu dhidi ya Malawi kabla kuivaa Ivory Coast ugenini Juni 2 mwaka huu jijini Abidjan.
 
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Sunday, May 13, 2012

Yametimia, Man City bingwa England

Raha ya ushindi
HATIMAYE Manchester City imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England ya EPL baada ya kuifunga QPR mabao 3-2 katika mchezo wa fungadimba huku Manchester United ikishinda lakini City wakijivunia idadi ya mabao ya kufunga.
Ilikuwa Jumapili nyepesi kwa City, kwani walikuwa wakicheza na timu nyepesi ya Queens Park Rangers ambao walifungwa kirahisi. Licha ya Rangers kucheza ikiwa na watu 10, ilipata mabao yake dakika za mwishoni yaliyoipa City heshima.
Ushindi huo uliacha mashabiki kutoa machozi kwa kushindwa kuaamini kilichotokea kwenye Uwanja wa  Etihad, City, iliyokuwa nyuma kwa mabao 2-1 na kushindwa kuipenya ngome ya QPR kwa dakika 51 walibadili upepo na kupata mabao hayo.
Edin Dzeko alifunga bao la kusawazisha kabla ya Sergio Aguero, alifunga na kufanya matokeo kuwa 3-2 kwa shuti la mguu wa kulia na City walianza kushangilia na Manchester kabla ya bao lingine kufungwa.
United, iliyoilaza Sunderland 1-0 na kufungana pointi na City 89, baada ya mpira kumalizika na wachezaji wa United na kocha wao walijipanga kwa ajili ya ubingwa, lakini mambo yalibadilika. Baadaye zilikuja taarifa kuwa Manchester watabakia wa pili kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Matokeo mengine England:-
Wachezaji wa Man City wakishangilia na kombe lao la ubingwa wa England kutwaa juzi.

Chelsea 2-1 Blackburn
Everton 3-1 Newcastle
Norwich 2-0 Aston Villa
Stoke 2-2 Bolton
Swansea 1-0 Liverpool
Tottenham 2-0 Fulham
West Brom 2-3 Arsenal
Wigan 3-2 Wolves