Wednesday, May 8, 2024

 MAKALLA AWAAMBIA HADEMA; KATIBA MPYA

SIO SAWA NA KUSONGA UGALI


Ripota, ZeNews

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA, Amos Makalla amewaambia Chadema kuwa hitaji la Katiba Mpya si sawa na kusonga ugali mara moja umeiva.

Makalla ameyasema hayo leo Mei 8, 2024 kwamba kila mara wapinzani hasa Chadema wamekuwa wakitaka Katiba mpya, na kwamba suala la Katiba ni mchakato.

Amesema Katiba Mpya si sawa na kusonga ugali kwamba unabandika maji, mara yamechemka, unaweka unga, unasonga na ugali tayari.

Makalla amesema Chadema wanapigia kelele Katiba Mpya wakati ndani ya chama chao hakuna demokrasia, na kwamba wangerekebisha katiba yao kwanza ndipo watoke kuzungumzia hili.

Itakumbukwa, Serikali ilitangaza miaka mitatu ya kutoa elimu ya Katiba kabla shughuli ya Katiba haijaanza.

Hata hivyo, Makalla amesema Chadema wangejiangalia kabla ya kudai Katiba kwani hata Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe amevunja katiba yao kwa kukaa muda mrefu kama kiongozi wa chama.

 

 



MAKALLA: TUTAWASHINDA CHADEMA KWA KISHINDO

 

Ripota, ZeNews Blog

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi, CPA Amos Makalla amesema chama chake kimejipanga na kitashinda uchaguzi wa Serikali za Mitaa na ule wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa kishindo.

Akizungumza leo Mei 8, 2024 kupitia Wasafi FM, amesema kama chama wamejipanga kila eneo na Chadema wataangushwa hadi watajishangaa kwa kipigo.

Amesema wamefanya utafiti ndani ya CCM  kwamba ushindi wa kishindo hauna mjadala na wameangalia maandalizi yaliyofanyika yanawapa nguvu kufanya vizuri.

Makalla amesema silaha kubwa ya ushindi katika uchaguzi wa mitaa,  ni utekelezaji wa ilani na Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa ikiwemo kupeleka fedha nyingi katika miradi mbalimbali mikubwa na midogo na kila mahali kuna alama.

Ameyataja baadhi ya maeneo yaliyoshughulikiwa kuwa ni eneo la umeme, maji, elimu, huduma za afya na kwamba kupitia utekelezaji wa ilani hiyo, CCM ina uhakika wa ushindi wa kishindo.

Aidha amesema ushindi mwingine watakaoupata utatokana na udhaifu unaoendelea sasa ndani ya Chadema kwani CCM ilidhani walikuwa wapinzani wa kweli, lakini wamebaini ni chama kinachokwenda kuporomoka.

Amesema kuporomoka kwa Chadema kunatokana na mgogoro mkubwa ulioko ndani ya chama hicho ikiwemo madai ya kukinzana; uenyekiti, urais, fedha chafu na hoja mbalimbali ambazo viongozi wakuu wanavutana na ndizo dalili mbaya.

Mbali na hayo amesema Chadema hawatakuwa na cha kuwaeleza wananchi kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa zaidi ya kuwaambia wamefanya maandamano.

Akikizungumzia chama chake, Makalla amesema wao wanawapa wananchi; matumani; wanawaandaa watu na kwamba Chadema hawajaonyesha nia ya dhati kushiriki uchaguzi wa mitaa kwa kuwa hawana cha kuwaambia wananchi.

Akisisitiza ushindi huo wa kishindo kwamba ni ushindi wa haki na kama chama kina kiongozi makini na ndiyo maana anakubalika.

Kitu kingine amesema CCM kufanya harakati kwa kuandaa watu na kuwaelezea kile kilichofanyika ikiwemo kujitathmini.

 

Sunday, December 28, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

LIGI KUU YA VODACOM YAINGIA RAUNDI YA 9

Wakati raundi ya nane ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inakamilika leo (Desemba 29 mwaka huu) kwa mechi tatu, ligi hiyo itaingia raundi ya tisa Januari 3 mwakani kwa mechi tano.

Coastal Union itacheza na JKT Ruvu katika Uwanja wa Mkwakwani, Ruvu Shooting itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mabatini, Azam itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Azam Complex, Stand United itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri wakati Mbeya City na Yanga zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Sokoine.

Ligi hiyo ambayo itachezwa mfululizo (non-stop) hadi itakapomalizika Mei 9 mwakani, itakamilisha raundi ya tisa Januari 4 mwakani kwa mechi kati ya Mgambo Shooting na Simba kwenye Uwanja wa Mkwakwani, na Tanzania Prisons itakayokuwa mwenyeji wa Ndanda kwenye Uwanja wa Sokoine.

Nayo mechi kati ya Mtibwa Sugar na Stand United ambayo jana ilivunjwa na mvua dakika ya 6 imemaliziwa leo ambapo timu hizo zimetoka sare ya bao 1-1.

Wakati huo huo, mechi ya ligi iliyochezwa jana usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex imemalizika kwa wageni Ruvu Shooting kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Ruvu. Bao hilo lilifungwa kipindi cha kwanza kwa mkwaju wa penalti uliopigwa na Hamisi Kasanga. 


MBAO FC YAKAMATA USUKANI SDL
Timu ya Mbao FC ya Mwanza imekamata uongozi wa Kundi B la michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) baada ya jana (Desemba 27 mwaka huu) kuizamisha JKT Rwamkoma ya Mara mabao 2-1.

Kwa matokeo hayo katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mbao FC imeitoa kileleni JKT Rwamkoma baada ya kufikisha pointi tisa kwa kushinda mechi zote tatu dhidi ya Arusha FC, Pamba na JKT Rwamkoma. 

Mbao FC inafuatiwa na JKT Rwamkoma yenye pointi sita, Arusha FC pointi sita wakati Bulyanhulu na Pamba zikiwa za mwisho kwa pointi moja kila moja. Kundi hilo litakamilisha mzunguko wa kwanza Januari 3 mwakani kwa mechi kati ya JKT Rwamkoma na Arusha FC, na Bulyanhulu na Mbao FC.

Katika kundi A, Mji Mkuu (CDA) na Singida United ndizo zinazochuana kileleni kwa kufikisha pointi saba kila moja. Timu hizo zinafuatiwa na Milambo yenye pointi nne, Mvuvumwa FC yenye pointi moja wakati Ujenzi Rukwa ni ya mwisho ikiwa haina pointi.

Hata hivyo, Mvuvumwa FC na Milambo ziko nyuma kwa mechi moja. Mechi hiyo ya kukamilisha raundi ya tatu kati ya timu hizo itachezwa kesho (Desemba 29 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

Kiluvya United imeendelea kuchachafya kundi C baada ya kushinda mechi zote ne ilizocheza, hivyo kufikisha pointi 12. Inafuatiwa na Mshikamano yenye pointi saba huku Abajalo ikiwa katika nafasi ya tatu kwa pointi 6.

Nafasi ya nne inashikwa na Transit Camp yenye pointi nne, Cosmopolitan yenye pointi mbili ni ya tano wakati Kariakoo ambayo haina pointi ni ya mwisho. Hata hivyo, Cosmopolitan na Kariakoo zina mchezo mmoja mkononi.

Mechi zinazofuata za kundi hilo ni Januari 3 mwakani kati ya Kariakoo na Mshikamano na Mshikamano (Ilulu), Transit Camp na Abajalo (Mabatini), na Cosmopolitan na Kiluvya (Karume).

Kundi D, vinara bado ni Njombe Mji yenye pointi 12 ikifuatiwa na Wenda yenye pointi sita wakati Volcano FC iko nafasi ya tatu ikiwa na pointi tano. Mkamba Rangers ina pointi nne, Town Small Boys ina pointi moja wakati Magereza FC haina pointi.

Katika kundi hilo leo (Desemba 28 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Town Small Boys na Magereza itakayochezwa Uwanja wa Majimaji mjini Songea. Januari 3 mwakani kutakuwa na mechi kati ya Town Small Boys na Njombe Mji, Volcano FC na Magereza, na Wenda na Mkamba Rangers.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
Wajumbe wa Baraza la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wilayaya Mlele, mkoani Katavi wakifurahi jambo na Mama Tunu Pinda wakati alipofungua mkutano wao katika Shule ya Sekondari ya Mamba Desemba 28, 2014. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Monday, December 8, 2014


Lowassa na askofu
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akimjulia hali Askofu Mkuu Katoliki Jimbo Kuu Tabora, Paul Ruzoka katika Hospitali ya TMJ Mikocheni Dar es Salaam leo. Picha na I.M.B.



THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

Telephone: 255-22-2114512, 2116898
Website : www.ikulu.go.tz              

Fax: 255-22-2113425


Coat of Arms
PRESIDENT’S OFFICE,
      STATE HOUSE,
              1 BARACK OBAMA ROAD,  
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais aanza kazi rasmi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatatu, Desemba 8, 2010, ameanza kazi rasmi baada ya afya yake kuimarika kufuatia upasuaji aliofanyiwa mwezi uliopita.
Mhe. Rais ameanza kazi rasmi kwa kumwapisha Mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Daudi Felix Ntibenda katika shughuli fupi iliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam.
Rais Kikwete katika moja ya majukumu ya kitaifa.
Kwa kuanzia Mhe. Rais atakuwa anafanya kazi za ofisini na kwa muda mchache. Muda na kasi ya kufanya kazi ya Mhe. Rais vitaongezeka kwa kadri afya yake inavyozidi kuimarika.
Na kwa sababu sasa ameanza kazi, Mhe. Rais ataanza kushughulikia mambo yale ambayo yamekuwa yanasubiri maamuzi yake.
Rais Kikwete alifanyiwa upasuaji wa tezi dume katika Hospitali ya Johns Hopkins ya Baltimore, Maryland, Marekani Novemba 8, mwaka huu na alirejea nyumbani Novemba 29, mwaka huu.
Tokea awasili nyumbani, Mhe. Rais amekuwa anafanya mazoezi asubuhi na jioni kuimarisha afya yake kama alivyoshauriwa na madaktari.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
8 Desemba,2014