MAKALLA: TUTAWASHINDA CHADEMA KWA KISHINDO
Ripota, ZeNews Blog
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
Chama cha Mapinduzi, CPA Amos Makalla amesema chama chake kimejipanga na
kitashinda uchaguzi wa Serikali za Mitaa na ule wa Rais, Wabunge na Madiwani
kwa kishindo.
Akizungumza leo Mei 8, 2024 kupitia
Wasafi FM, amesema kama chama wamejipanga kila eneo na Chadema wataangushwa
hadi watajishangaa kwa kipigo.
Amesema wamefanya utafiti ndani ya
CCM kwamba ushindi wa kishindo hauna
mjadala na wameangalia maandalizi yaliyofanyika yanawapa nguvu kufanya vizuri.
Makalla amesema silaha kubwa ya
ushindi katika uchaguzi wa mitaa, ni
utekelezaji wa ilani na Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa ikiwemo
kupeleka fedha nyingi katika miradi mbalimbali mikubwa na midogo na kila mahali
kuna alama.
Ameyataja baadhi ya maeneo
yaliyoshughulikiwa kuwa ni eneo la umeme, maji, elimu, huduma za afya na kwamba
kupitia utekelezaji wa ilani hiyo, CCM ina uhakika wa ushindi wa kishindo.
Aidha amesema ushindi mwingine watakaoupata
utatokana na udhaifu unaoendelea sasa ndani ya Chadema kwani CCM ilidhani
walikuwa wapinzani wa kweli, lakini wamebaini ni chama kinachokwenda
kuporomoka.
Amesema kuporomoka kwa Chadema
kunatokana na mgogoro mkubwa ulioko ndani ya chama hicho ikiwemo madai ya
kukinzana; uenyekiti, urais, fedha chafu na hoja mbalimbali ambazo viongozi
wakuu wanavutana na ndizo dalili mbaya.
Mbali na hayo amesema Chadema hawatakuwa
na cha kuwaeleza wananchi kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa zaidi ya
kuwaambia wamefanya maandamano.
Akikizungumzia chama chake, Makalla
amesema wao wanawapa wananchi; matumani; wanawaandaa watu na kwamba Chadema
hawajaonyesha nia ya dhati kushiriki uchaguzi wa mitaa kwa kuwa hawana cha
kuwaambia wananchi.
Akisisitiza ushindi huo wa kishindo
kwamba ni ushindi wa haki na kama chama kina kiongozi makini na ndiyo maana
anakubalika.
Kitu kingine amesema CCM kufanya
harakati kwa kuandaa watu na kuwaelezea kile kilichofanyika ikiwemo
kujitathmini.