Saturday, December 6, 2014
Hotuba ya Sumaye Arusha leo
TAASISI YA UELIMISHAJI VIJANA WA SEKONDARI NA VYUO VIKUU
HOTUBA YA MGENI RASMI MHE. FREDERICK T. SUMAYE WAKATI WA KUFUNGUA SEMINA ELEKEZI YA UHAMASISHAJI
MAHALI: UKUMBI WA CCM MKOANI ARUSHA
TAREHE: 06 DESEMBA, 2014
Ndugu ... Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha,
Ndugu Nickson Mmanyi, Mwenyekiti wa Taasisi,
Ndugu Hassan Joari, Katibu Mtendaji wa Taasisi,
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Arusha,
Baba Askofu,
Ndugu zangu Wajumbe wa Mkutano,
Ndugu Wanahabari,
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Shukurani
Napenda niwashukuru sana viongozi wa Taasisi hii ya kuwaelimisha vijana juu ya mambo mbali mbali kwa kunialika kuwa mgeni rasmi katika semina hii ya uhamasishaji wa vijana juu ya majukumu mbali mbali waliyonayo na yale yanayowapasa. Asanateni sana kwa heshima kubwa mliyonipa.
Pili, napenda kuwapongeza sana viongozi kwa jinsi walivyosimamia shughuli kwa ufanisi mkubwa pamoja na mazingira magumu wanayokumbana nayo. Hongereni sana.
Tatu, napenda kwa niaba ya viongozi wa Taasisi niwashukuru wote ambao kwa njia moja au nyingine wamewasaidia hawa vijana katika juhudi yao ya kufanikisha semina hii, na hao ni pamoja na Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha.
Madhumuni ya semina
Semina hii itashughulikia mambo matatu muhimu kwa vijana na kwa nchi yetu kwa ujumla. Mambo hayo ni pamoja na:
· Nafasi ya vijana katika kulinda amani, usalama na utulivu wa nchi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015
· Ujasirimali kwa vijana
· Mikopo kwa wananfunzi wa vyuo vikuu na wa shule za sekondari.
Hoja hizi zote ni muhimu sana kwa mustakabali wa taifa letu na maendeleo ya jamii kwa ujumla wake. Najua kuna mada zitakazotolewa juu ya hoja hizi na wataalam waliobobea lakini na mimi nigusie tu juu ya baadhi.
Nafasi ya vijana katika kulinda amani, usalama na utulivu wa nchi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
1) Mambo yanayoathiri amani na utulivu
Kwanza ili vijana hawa wawe walinzi wazuri wa amani, usalama na utulivu ni vema tukajikumbusha ni vitu au matendo gani yanayoweza kusababisha uvunjivu wa amani hasa wakati wa uchaguzi.
· Siasa za chuki – ni vema vyama vya siasa vikaelewa kuwa nchi yetu iko katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, hivyo ni halali na haki kama kundi la watu wataanzisha chama cha siasa kwa kufuata taratibu na sheria inayohusika. Vyama vione kuwa kila moja ni mshindani wa mwenzake na siyo adui wa mwenzake. Ni nini basi nafasi ya vijana katika kusimamia jambo hili? Vijana ndiyo mara zote wanaotumika na vyama vya siasa ili kupambanisha na vijana wa chama au vyama vingine. Ni vema vijana mkaepuka hili la kutumika vibaya na vyama vya siasa na badala yake ninyi ndiyo mkawa wa kuzuia na kukemea vitendo vya aina hiyo. Fujo haijengi bali hubomoa misingi ya amani na utulivu wa nchi.
· Vyama vya siasa na wafuasi wao kutotii sheria na taratibu zilizowekwa kwa ajili ya mchakato mzima wa kampeni ikiwa ni pamoja na ratiba za kampeni na utaratibu mzima wa upigaji kura. Kuna vyama vya siasa ambavyo vikishagundua kuwa haviwezi kushinda basi huleta fujo katika katika mchakato wa kampeni nap engine huleta fujo hata kuwaumiza wafuasi wa chama kingine. Hapa napo vijana hutumika katika hujuma hizo zinazovunja amani na utulivu katika chaguzi zetu na nchi kwa ujumla.
· Haki sawa kutokuonekana kutendeka kwa vyama vyote vya siasa. Hili ni jambo la hatari sana kwa amani na usalama wa nchi. Wakati wa uchaguzi ni lazima wahusika wote hasa tume ya uchaguzi lazima itende na ionekane inatenda haki sawa kwa kila mgombea wa kila chama. Upendeleo na uonevu wa aina yoyote iwe baina ya vyama au baina wagombea ni sumu kwa amani na utulivu wetu.
· Kutokuwa na uwazi wa kutosha katika shughuli zote zihusuzo uchaguzi hasa wakati wa kuhesabu kura na kutangaza matokeo. Hisia yoyote ya udanganyifu, upendeleo au uwizi wa kura ni sumu ya amani na utulivu. Uchaguzi ndipo mahali ambapo raia hutumia haki yake ya kuchagua na kuchaguliwa na hiyo haki yake ya msingi. Jambo lolote linalotafsiriwa kupokonya haki hii haitavumiliwa na hujibiwa kwa mapambano. Nchi nyingi hupoteza amani na utulivu wao katika hatua hii ya mchakato wa kura.
· Kukataa matokeo. Nchi nyingi zimejikuta katika uvunjivu wa amani na utulivu kunapokuwa na chama au upande moja unaokataa matokeo ya kura zilizopigwa. Mifano ya hali hii ni mingi katika nchi za Afrika na mara kadhaa serikali zimeangushwa au kuishia katika mgawanyo wa madaraka jambo ambalo linawanyima raia haki ya kutetewa bungeni na upande wa upinzani ambao katika utaratibu huo nao huingia katika serikali ya mseto. Kuna wakati mwingine upande pinzani hukataa matokeo hata kama ni ya halali. Ni vema pale ambapo udhalimu haukutumika katika uchaguzi, vyama vyetu vikajua kuwa asiyekubali kushindwa si mshindani na hakuna utaratibu ambao unawafanya washindani wote kuwa washindi.
· Rushwa katika uchaguzi. Hili ni janga la demokrasia. Katika uchaguzi watu hutumia haki yao ya kuchagua kiongozi wamtakaye. Rushwa kama tujuavyo ni adui wa haki, kwa hiyo rushwa na uchaguzi wa haki haviwezi kuishi pamoja. Penye rushwa hakuna uchaguzi wa haki. Rushwa hapa ziko za aina kadha ambazo zote huathiri na kupoteza maana ya uchaguzi wa haki. Wako wanaotoa fedha ili kuwarubuni wapiga kura hivyo huwanunua wapiga kura kama bidhaa za sokoni. Mara nyingi watu hawa hutumia fedha nyingi sana ambazo hata hazijulikani zinatoka wapi na wakipata huo uongozi wanaoununua hizo fedha za watu zinarudije. Hawa mara nyingi wao wenyewe ni ama wala rushwa, ama wezi wa mali ya umma au wauza madawa ya kulevya. Vinginevyo hizo fedha nyingi namna hiyo wangezitoa wapi. Tatizo lingine linalofuatia mara baada ya hapo kama atakuwa amefanikiwa kuununua huo uongozi, basi kazi yake ya kipaumbele ni kuongeza kasi na viwango vya hiyo rushwa, uwizi wa mali umma au uuzaji wa madawa ya kulevya ili kurudisha fedha zake alizohonga nazo wapiga kura na faida kubwa juu yake. Hali hii huweka madarakani utawala mbovu na haki hutoweka kabisa katika nchi. Haki ikishatoweka haiwezekani kukawa na amani na utulivu.
2) Nafasi ya Vijana
Vijana wana maslahi makubwa zaidi ya kuona kuwa nchi inakuwa katika hali nzuri ya maendeleo kuliko makundi mengine ya jamii. Hii ni kwa sababu vijana ndiyo wakaokaa katika nchi yao kwa muda mrefu zaidi hivyo ni lazima wapende kuishi katika nzuri ya baadaye. Vijana wanayo nafasi nzuri nay a wazi kutengeneza mazingira hayo ya kutengeneza nchi ya ndoto yao wakipenda. Lakini vijana pia wanayo nafasi ya kuiharibu nchi au kujitengenezea nchi ya hovyo ya baadaye.
Vijana wanayo nafasi na uwezo wa kujijengea nchi nzuri watakayoipenda kwa kufanya mambo kadha ili nchi iwe na amani na utulivu, nitataja tu machache.
· Kujenga uzalendo wa kweli kwa nchi yetu na kwa Watanzania. Inaonekana uzalendo unaanza kuwa bidhaa adimu katika nchi yetu. Vijana lazima muwe mstari wa mbele kulitambua hili na kusimamia maadili ya kujenga uzalendo wa kweli kwa watu wote. Kupoteza uzalendo ndiyo kunakosababisha watu kuwa waporaji wa mali umma bila huruma, kukosa uzalendo ndio kunakosababisha watu kula rushwa bila kujali kuwa kwa kufanya hivyo wanadhulumu haki za wengine, kukosa uzalendo ndiko kunakowafanya watu kufisadi mali ya uma bila kujali kuwa kwa kufanya hivyo nchi inaingia katika hasara kubwa na wananchi wanakosa huduma muhimu ambazo zingetengenezwa na mradi uliofisadiwa, kukosa uzalendo ndiko kunakosababisha watu kuwafanya watoto wa wenzao makontena yao ya kubebea madawa ya kulevya.
· Kuweka madarakani serikali nzuri itakayosimamia maslahi ya umma na siyo maslahi binafsi. Tatizo kubwa sana katika nchi nyingi zinazoendelea hasa nchi za Afrika ni Uongozi Dhaifu na Utawala Mbovu. Kama hatutaweka madarakani viongozi wenye uzalendo wa kweli kwa nchi na watu wake, wenye uchungu na nchi na watu wake, na badala yake tukaweka wabinafsi, kama hatutaweka madarakani viongozi waadilifu na watenda haki na badala yake tukaweka wala rushwa au watoa rushwa, kama hatutaweka madarakani viongozi wachapa kazi na wenye dira ya kutuongoza watanzania na badala yake tukaweka wababaishaji; hatuwezikujenga nchi imara kiusalama na amani.
· Kushiriki katika shughuli muhimu za uchaguzi. Huko nyuma tumekuwa na tatizo la vijana wengi kutokujiandisha kupiga kura na baada ya uchaguzi hubaki kulalamika kuwa viongozi waliopo siyo wazuri. Kama hukushiriki kuchagua kiongozi wako itabidi upokee waliyekuchagulia wenzako na wala usilalamike tena. Kama nilivyoeleza awali kuwa vijana lazima muweke madarakali serikali itakayowajibika kwa umma, huwezi kufanya hivyo kama hujajiandikisha kama mpiga kura. Kwa hiyo natoa wito kwa vijana wote wao wenyewe kujiandikisha kupiga kura na kwenda kupiga kura siku ya kupiga kura. Aidha vijana mnalo jukumu kubwa la kuwaelimisha umma nao kujiandisha kupiga kura na kwenda kupiga kura. Katika elimu hiyo ni muhimu wananchi wakaelimishwa madhara ya rushwa katika chaguzi zetu. Kura ni haki ya msingi sana ya mwanchi ambayo akiitumia vizuri atajiletea maendeleo na akiitumia vibaya kwa kuweka wala rushwa na mafisadi au wenye mapungufu mbali mbali, basi ajue amejinunulia au kujiwekea majanga ya maendeleo yake.
· Kuwa mfano wa tabia njema katika jamii. Ili kudumisha amani na utulivu, vijana lazima wawe askari wema na watiifu wa jamii ambao wako tayari kupambana na maovu yote katika jamii yao. Vijana wasiwe askari wa kukodiwa au mamluki bali wawe askari waaminifu wa jamii. Vijana wawe ndiyo chachu ya maendeleo kwa sababu ndiyo nguvukazi ambayo jamii inaitegemea. Kwa ujumla vijana wakiwa washiriki wa mambo mema na wapinga mambo yote mabaya jamii itaishi katika amani na utulivu wa uhakika siyo nyakati za uchaguzi bali nyakati zote.
Mwisho
Kama tulivyoona vijana mnayo nafasi kubwa kuliko kundi lolote la kutengeneza nchi muitakayo kwa maisha yenu ya baadaye mkitumia karata zenu vizuri hasa wakati wa uchaguzi na fursa hiyo mnaweza kuitumia kwa kuanzia uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Nawatakieni utekelezaji mwema wa haya yote na yote mtakayoelezana katika semina yenu elekezi.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment