Thursday, December 4, 2014

SBL Yafungua Ghala Mbeya
 
Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) imefungua ghala lake kubwa la kwanza Mkoani Mbeya lenye uwezo wa kuhifadhi masanduku 80,000 mpaka 100,000 ya bia kwa ajili ya kuhifadhi na kusambaza bidhaa zake kwa wateja wake wote wa ndani na nje ya nchi.
 
Hayo ni mafanikio makubwa kwa SBL yaliyopatikana hivi karibuni katika nusu ya kwanza ya mwaka 2014. Ufunguzi wa ghala hilo utaleta mafanikio makubwa katika uendeshaji wa shughuli za SBL pamoja na kugusa maisha ya watu waliopo katika shughuri mbalimbali za uendeshaji wa SBL.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Bw. Steven Gannon alisema ghala hilo litaongeza uwezo wa kampuni kuzalisha bidhaa zake kwa wingi kwa wateja wake wa mikoa ya nyanda za juu kusini ambayo ni Mbeya, Rukwa, Iringa na Ruvuma. Ghala hilo litasaidia kuweka akiba ya kutosha ya bia tofauti na hapo awali.
 
“Katika msimu huu wa Siku Kuu ya Krismasi na Mwisho wa Mwaka tunauhakika wa kukidhi mahitaji ya wateja wetu. Kila mtu atakunywa mpaka atakaporidhika na kwa ustaarabu,’’ alisema Bw. Gannon.
 
“Ufunguzi wa ghala hilI kwa kiasi kikubwa utapunguza gharama za usafirishaji kwa upande wa wasambazaji wetu  na kuongeza manunuzi zaidi. Hii itapunguza gharama zao za  muamala na hivyo kupata faida zaidi kwa kushirikiana na SBL,” aliongeza kusema Bw. Gannon.
 
Ufunguzi wa ghala hilo pia utatoa fursa zaidi za ajira katika nyanja mbalimbali za shughuli za SBL kama vile madereva, mafundi magari, mamalishe, makarani na kuongeza idadi ya wasambazaji.
“Matokeo ya mwisho ambayo ni muhimu zaidi kuliko yote kwa kufunguliwa ghala hili ni kuongezeka kwa mauzo kwa kampuni ya SBL, kwani wasambazaji zaidi kutoka nyanda za juu kusini watavutiwa kujiunga na biashara yetu kutokana na upatikaji huduma hiyo kwa urahisi,” alisema Bw. Gannon.
 
Mafanikio mengine ya SBL ni kwamba Novemba 23, 2014 walisherehekea kutimiza siku ya 1000 bila kupata ajali katika kiwanda cha SBL cha Mwanza, ambapo hiyo ni rekodi ya kwanza kuwekwa Tanzania na ya pili kwa Diageo.
 
Naye mgeni rasmi, Norman Sigalla alisema  ufunguzi huo ni hatua muhimu katika juhudi za kampuni ya SBL ya kuleta huduma zake karibu na wateja wake. Alisema hiyo ni hatua muhimu kwa watumiaji wa bidhaa hizo katika mikoa ya Nyanda za Juu kusini kwani sasa kutakuwa na upatikanaji wa uhakika na kwa muda wowote wa bidhaa za SBL.
 
Bw. Sigalla alisema Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini itanufaika na ufunguzi huo kwa sababu mawakala wa bidhaa za SBL walikuwa wanalazimika kwenda umbali mrefu kutafuta bidhaa hizo hivyo kuwaongezea gharama za uendeshaji. Jambo hilo lilipunguza sana soko la bidhaa za SBL katika maeneo hayo.
 
Mkuu wa Wilaya alisema kitendo hicho kilimnyima mteja/mnywaji haki yake ya msingi ya kuchagua kinywaji akipendacho, kwani alilazimika kunywa kile kinachopatikana kwa wakati huo.
 
Bw. Sigalla alisema Serikali inatambua mchango mkubwa utolewao na SBL kwa wakulima wa shayiri na mahindi katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, akisema kwa kuingia nao mikataba ya kununua mazao yao wanafaidika kwa namna nyingi.
 
Alisema kipato cha uhakika wanachopata kutoka SBL kinawawezesha wakulima hao kumudu gharama mbalimbali za maisha kama vile kulipa karo za watoto wao wanaosoma, kulipia huduma za hospitali na mahitaji mengine muhimu.
 
Mkuu huyo wa Wilaya aliuomba uongozi wa SBL kufikiria kujenga kiwanda mkoani Mbeya ili kuongeza kasi ya ukuaji uchumi na kuongeza ajira kwa watu wenye sifa katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
 

No comments:

Post a Comment