Sunday, March 25, 2012

Daktari wa Villa Squad aaga dunia

ALIYEKUA Daktari mkuu wa timu ya soka ya Villa Squad Fc ‘Kambimoto’ Nassoro Mahmoud amefariki dunia alfajiri ya kuamkia jana alipokua amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kufuatia kusumbuliwa na maradhi ya muda mrefu na kutarajiwa kuzikwa jioni ya leo kijijini kwake Mbwewe,Tanga.
Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Ofisa Habari wa Villa, Andrew Chale alisema kua Dkt Nassoro alikua akisumbuliwa ugonjwa kwa muda mrefu ikiwemo kifua na kupewa mapumziko na timu yake takribani miezi miwili iliyopita mpaka alfajiri ya jana alipopatwa na umauti.
“Villa tumeupokea msiba huu mzito wa daktari wa timu ambaye alikua muhimiri kwa Villa ni majonzi makubwa kwa kipindi hichi tutaendelea kumuezi daima na kukumbuka mchango wake” Alisema Chale kwenye taarifa hiyo.
Mwenyekiti wa Villa, Alhaji Ramadhan Uledi, alisema habari za kifo hicho kimemshtua sana kwani kimekuja wakati mgumu kwa timu hiyo ambayo kwa sasa ipo chini kwenye msimamo wa ligi hivyo kuendelea kuwaumiza na majonzi makubwa.
Daktari Nassoro alikuwa akitambuliwa na shirikisho la soka TFF na chama cha madaktari wa michezo Tasma kwa nyadhifa yake hiyo ya Udaktari wa timu na alikua akishirikiana na madaktari wenzake wa timu nyingine ikiwemo kutoa ushahuri wa kitiba.
Mwisho

No comments:

Post a Comment