Tuesday, March 27, 2012

Kombe la UEFA hadharani Tanzania

Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya, UEFA
KOMBE la Ligi ya Mabingwa Ulaya, limewekwa hadharani kwenye Hoteli ya Kilimanjaro Kempinsky na kila mmoja alipiga nalo picha kama sehemu ya ukumbusho.
Mamia ya wageni waalikwa, walipiga nalo picha katika hafla iliyokuwa imechangamka na kudhaminiwa na kampuni ya bia ya Heineken ambao ndiyo wadhamini wakubwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kabla ya kufunuliwa hadharani na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk. Fenella Mukangala, Kombe hilo lililokuwa linatokea Mexico na kutua nchini kupitia Kilimanjaro International Airport
Wakati Kombe lililokuwa limefunikwa kitambaa cheupe likifunuliwa, wimbo maarufu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ulikuwa ukipigwa na kupokewa kwa mashamsham huku fataki zikipigwa nje ya hoteli hiyo na kufanya anga za hoteli hiyo kupendeza.
Mapema, Mukangala aliwataka vijana wenye vipaji kujituma katika mazoezi waweze kusajiliwa na timu kubwa za Ulaya ili nao siku moja waweke historia kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Fenella aliyasema hayo juzi usiku kwenye Hoteli ya Kempinsky wakati wa kulionyesha Kombe la Ulaya (Ligi ya Mabingwa) hadharani.
Moja ya mechi za Ligi ya Mabingwa, Barca vs Panathinaikos
Alisema kuwa ujio wa kombe hilo si tu kwa ajili ya kulitazama, bali ni changamoto kwa vijana wacheze mpira, kujituma ili nao wapate nafasi ya kucheza soka Ulaya na kupata tiketi ya kucheza kombe hilo.
Dk. Fenella pia alitumia nafasi hiyo kuwataka Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, kuandaa mashindano mengi yanayofanana na Uefa hasa kwa timu za vijana ili iwe changamoto kwao.
Mbali na hayo, aliwataka wadhamini wa michuano hiyo ya Uefa Kampuni ya Bia ya Heineken kuidhamini timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars kwani ni moja ya timu zinazopiga hatua katika maendeleo ya soka.
"Ningependa kuwashauri Heineken kujikita zaidi katika kudhamini soka Tanzania na hasa soka ya wanawake pamoja na kuidhamini Twiga Stars na pia kuangalia maendeleo ya soka kwa vijana.
"Sisi kama serikali tuitakuwa pamoja na tunataka kuona kunakuwepo na ustawi wa soka kwa vijana ambao ndiyo msingi wa maendeleo husika," alisema Fenella ambaye aliwashukuru waandaaji wa ziara hiyo kwa kukubali kulileta kombe Tanzania.
Kombe hilo lililotokea Mexico liliingia nchini Jumamosi iliyopita na linaondoka  Jumatano kwenda Kenya na baadaye kuendelea na ziada yake nchini China.
Meneja wa Heineken Afrika Mashariki, Koen Morshuis alisema kuwa Tanzania imeteuliwa kama nchi ya kwanza Afrika kufikiwa na kombe hilo kwa kuwa ina mashabiki wengi wanaofuatilia michuano ya Uefa ikifutiwa na Kenya.
mwisho

No comments:

Post a Comment