Saturday, March 10, 2012

Vua kiatu kupigwa 'live' U/Taifa Aprili 8

Anastazia Mukabwa
WIMBO wa mwanamuziki mashuhuri kutoka Kenya, Anastazia Mukabwa, 'Kiatu chako kivue' utapigwa live kwenye Uwanja wa Taifa Aprili 8, ikiwa ni sehemu ya Tamasha la Pasaka la nyimbo za injili.
Anastazia Mukabwa mwenye maskani yake nchini Kenya, alithibitisha kushiriki tamasha hilo ikiwa ni msanii wa kwanza kutoka nje ya Tanzania kufanya hivyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama alisema Dar es Salaam jana kuwa Mukabwa aliyeimba kwa kumshirikisha Rose Muhando katika wimbo huo, ameahidi kukonga nyoyo za mashabiki.
"Mpaka sasa tunaendelea na mazungumzo na waimbaji mahiri wa muziki wa Injili, wa ndani na nje ya Tanzania...Mukabwa amethibitisha kushiriki na ataambatana na kundi la wanamuziki wake wanane," alisema Msama.
Mukabwa bado anatamba na albamu ya Vua Kiatu na sasa yuko kwenye mazoezi makali kujiandaa kufanya mambo makubwa.
Albamu ya Vua Kiatu ina nyimbo nane ambazo ni Vua Kiatu uliobeba jina la albamu hiyo, Ee Mungu, Usiwe Manamba, Nzizilela, Nishike Mkono Bwana, Wanaokudharau na Mfalme.

No comments:

Post a Comment