Saturday, March 24, 2012

Sitta: Viongozi wabovu wameua michezo

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema viongozi wanaoingia madarakani kwa mgongo wa rushwa, kutumia miti shamba na wenye mlengo fulani, ndiyo walioifikisha michezo hapa ilipo.
Samuel Sitta
Sitta aliyasema hayo leo alipokuwa akizngumza na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali katika Bonanza la Waandishi wa habari, lililofanyika kwenye ufukwe wa Msasani na kuandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo, TASWA.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali na kuandamana na michezo, Sitta alisema Tanzania imekuwa nyuma katika kila mchezo na hiyo ni kutokana na kuwa na viongozi wasiokuwa na dira.
"Tuko nyuma sana, katika soka hali ni mbaya, riadha kidoogo, lakini ngumi, kikapu na mwaka jana nilikuwa mgeni rasmi pale Uwanja wa Ndani wa Taifa katika fainali, ikawa mbaya, haiwezekani Watanania mil45 tukose watu wenye vipaji.
"Haiwezekani vinchi vidogo kama Afrika ya Kati, Chad waibuke na kuonekana zinatisha kuliko sisi, sasa ninyi waandishi wapasheni, msiwe watu wa kutupaka mafuta.
"Wamulikeni viongozi wasiowajibika, hawa ndiyo hao walioingia kwa mipango na wameingia kwenye vyama vya michezo kwa kutarajia vitu fulani na ndiyo hao wanatumia rushwa, fedha na mambo mengine ali mradi waingie madarakani na matokeo yake michezo imepoteza mwelekeo.
"Tunachotaka ni kuona michezo inapiga hatua na zaidi kuwekeza katika michezo na kama kutakuwa na viongozi wabinafsi, kamwe michezo haiwezi kusonga mbele," alisema.
Awali, Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto, aliomba serikali kwa kushirikiana na TFF kukubalia siku moja kuwa mwenyeji wa Fainali za Afrika.
"Tunafahamu kuwa ni ghali, kuna mambo mengi, lakini ikijipanga, Tanzania inaweza kuwa mwenyeji siku moja kwani fainali za Afrika zitasaidia kutangaza nchi na tunaweza kutumia fainali hizo kwa kutangaza utalii wetu," alisema Pinto.

Soma zaidi www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment