Simba ya Dar es Salaam, imeichapa Azam FC mabao 2-0 katika mechi kali ya Ligi Kuu iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo iliyokuwa na kila aina ya mashamsham, ilianza kwa Azam kulishambulia lango la Simba ambao wamerudi kileleni kwa kufikisha pointi 37 huku Yanga ikiendelea na nafasi yake ya pili kwa kuwa na pointi 34 wakati Azam inabaki na pointi zake 32.
Mchezo wa leo ulikuwa wa ubabe, kila timu ilikuwa ikicheza kitemi, lakini Simba ndiyo walikuwa wa kwanza kuandika bao dakika ya 10, lakini mwamuzi alilikataa kwa madai mfungaji alikuwa ameotea.
Dakika ya 30, Emmanuel Okwi aliwanyanyua mashabiki wa Simba kwa kufunga bao safi na kumwacha kipa wa Azam, Mwadin Ally akiwa hana la kufanya.
Okwi alipachika bao la pili dakika 70 baada ya kutanguliziwa mpira wa kichwa na Felix Sunzu ambaye hata hata hivyo, baadaye aliumia na kutoka.
Kocha wa Azam, Stewart Hall aliwalaumu wachezaji wake kutokuwa makini na mchezo, lakini akasema ndivyo soka ilivyo wakati mwenzake wa Simba aliwapongeza wachezaji wake kwa kazi nzuri.
Mbali na matokeo hayo, Toto African ilitoka suluhu na Moro United wakati Villa Squad iliifumua Polisi Dodoma kwa kuichapa mabao 2-1.
Mechi nyingine, Coastal Union iliifunga African Lyon bao 1-0 kabla ya JKT Olchoro kuwafunga wenzao wa Ruvu bao 1-0.
No comments:
Post a Comment