<><>
<>

<><>

Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka, limefungua milango kwa wadau mbalimbali
kudhamini tamasha hilo linalowakusanya watu wengi wa dini mbalimbali.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa tamasha hilo, Alex Msama, alisema kuwa, kamati yake itakuwa tayari kupokea udhamini kutoka kwa mtu ama kampuni yoyote bila ya kubagua.

"Lengo la kuomba udhamini, ni kutaka kufanikisha tamasha hilo la kimataifa, kwani maandalizi yake ikiwemo kuwagharamia waimbaji ni kubwa sana," alisema.

Msama alisema kuwa, tamasha hilo litapokea udhamini kutoka kwa dini zote, kwani lengo lake ni kumtukuza Mungu kupitia nyimbo za injili.

Alisema pia wafanyabiadhara ambao watajitokeza kudhamini tamasha hilo, watapata baraka kubwa katika biashara zao na familia zao.

Mpaka sasa, baadhi ya waimbaji nyota wa ndani na nje ya nchi wameanza kuomba kushiriki, ambapo kamati ya tamasha hilo itakutana kupitia maombi yao na kuwatangaza.

"Tayari baadhi ya waimbaji nyota wa ndani na wale wa nje waliopelekewa mialiko wameanza kuthibitisha kushiriki, lakini kamati ndiyo itakayotangaza majina hayo," alisema.

Msama alisema baada ya kupokea maombi kutoka kwa wadau wa tamasha hilo kutafuta sehemu kubwa ya wazi, kamati imeanza mchakato ambapo wakifanikiwa, wataitangaza.

Mwenyekiti huyo wa tamasha alisema kuwa, tamasha la mwaka huu linatarajiwa kuwa la
kimataifa zaidi kwa kuwashirikisha waimbaji kutoka nje ya nje.

"Bado tunapokea maoni kutoka kwa wadau wetu, tunaomba mzidi kututumia ili tuyafanyie kazi kabla ya tarehe ya tamasha hilo," alisema.

Tamasha la Pasaka mwaka huu litafanyika Aprili 8, mwaka huu jijini Dar es Salaam,kabla ya kwenda mikoani.