Tuesday, February 7, 2012

Wadau waipa shavu Basata

BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limepongezwa na wadau wa Sanaa kwa juhudi zake katika kusimamia na kuratibu matukio mbalimbali ya Sanaa hapa nchini na kuyafanya kudumu.
Pongezi hizo zimetolewa wiki hii na wadau wa Sanaa wakati wakichangia mjadala uliohusu miaka mitano ya shindano la miss utalii na sanaa ya urembo nchini kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kwenye Ukumbi wa BASATA uliopo Ilala, Sharif Shamba.
Akizungumza wakati akieleza historia za shindano hilo, Rais wa Miss Utalii, Gideon Chipungahelo alisema kuwa, BASATA imekuwa bega kwa bega na shindano hilo katika kuhakikisha miongozo na kanuni mbalimbali za kuendesha mashindano zinafuatwa na kusisitiza kuwa, hiyo ndiyo sababu ya shindano hilo kuweza kupata baadhi ya mafanikio ya ndani na nje ya nchi.
“Naishukuru Serikali na BASATA, kila mara wamekuwa wakitoa maelekezo na miongozo ambayo imelifanya shindano hili kufikia mafanikio haya ingawa kumekuwa na changamoto kadhaa hasa za kukosa wadhamini” alisistiza Chipungahelo.
Aliongeza kuwa, BASATA imekuwa mara kwa mara ikikutana na kamati ya miss utalii na kuipa maelekezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya tathimini na wadau wa sanaa ya urembo ambao wamekuwa wakitoa michango ya kuliboresha shindano hilo.

No comments:

Post a Comment