Monday, February 6, 2012

TOC wanoa makocha wa ngumi

Mwandishi Wetu, Kibaha
KAMATI ya Olimpiki Tanzania, TOC, imelitaka Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania, BFT, kuueneza mchezo huo katika mikoa mbalimbali kwani kufanya hivyo kutainua mchezo huo.
Hayo yalisemwa na Katibu wa TOC, Filbert Bayi wakati akifungua mafunzo ya makocha ngumi za ridhaa, yanayofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Shule za Filbert Bayi, Kibaha mkoani Pwani.
Mafunzo hayo yameandaliwa na TOC kwa kushirikiana na Kamati ya Misaada ya Olimpiki, Olympic Solidarity, OS, ambayo ina kazi ya kuendesha mafunzo na misaada mbalimbali kuhusiana na michezo mbalimbali.
Bayi alisema kuwa BFT wana kazi ya ziada kuinua na kuueneza mchezo huo na kuachana na dhana ya kuutegemea mkoa wa Dar es Salaam ama mashindano kufanyika mkoani humo pekee.
"Bado BFT wana kazi ngumu, ngumi zimekuwa zikipiganwa mkoa wa Dar es Salaam na hasa katika majeshi...yakifanyika mashindano, ni mikoa michache inashiriki na kutoa nafasi ndogo ya ushiriki.
"Naomba kuchukua nafasi hii kuwashauri viongozi wa BFT kuueneza mchezo huu mikoani na mikoani ndiko kwenye wachezaji na vipaji vingi kuliko kuliko kutegemea klabu zilizoko mjini pekee," alisema.
Kwa muda mrefu, Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa, IOC, imekuwa ikitoa mafunzo ya utaalam kwa makocha mbalimbali ikiwemo wa ngum kwa kuwa mchezo huo ni miongoni mwa michezo inayoshindaniwa katika Michezo ya Olimpiki.
"TOC na IOC zinataka kuona ngumi zinapiga hatua na ndiyo maana zinatoa mafunzo kwa kuleta wataalam...ni gharama kuleta makocha lakini wanapopatikana wataalamu, tutumie mafunzo kuwapa walimu wenye taaluma na watutengenezee vijana.

No comments:

Post a Comment