Thursday, February 23, 2012

Upendo Kilahiro kupanda jukwaani Tamasha la Pasaka

Upendo Kilahiro
MWIMBAJI nguli wa muziki wa Injili mwenye sauti nyororo,
Upendo Kilahiro amekuwa wa kwanza kuthibitisha kushiriki
katika tamasha la Pasaka litakalofanyika Sikukuu ya Pasaka
 Aprili 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex

 Msama ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Msama
Promotions, alisema Dar es Salaam kuwa Kilahiro
amemthibitishia kwamba atashiriki tamasha hilo.

"Kilahiro tutakuwa naye kwenye tamasha, na naamini kwamba
 mwaka huu tamasha hili litakuwa bora zaidi kutokana na
 kushirikisha waimbaji wengi wakali," alisema Msama.
 Kwa mujibu wa Msama, tamasha hilo la aina yake, baada ya
kufanyika Dar es Salaam, pia litarindima kwenye Uwanja wa
 Jamhuri mjini Dodoma Aprili 9.
 Tamasha la mwaka huu malengo yake makubwa ni kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasomesha watoto yatima na kuwasaidia > mitaji wanawake wajane.
 Tamasha la Pasaka la mwaka huu litashirikisha waimbaji wa  nyimbo za Injili kutoka nchi kadhaa za Afrika ikiwa ni  pamoja na Kenya, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya
 Congo, Afrika Kusini na Zambia.
 Akizungumza Dar es Salaam, Kilahiro alisema amepania kufanya mambo makubwa katika tamasha la mwaka huu, na atapanda  jukwaani kuimba 'live' na bendi yake ya Upendo Kilahiro.
 "Natoa mwito kwa mashabiki wangu wasiwe na wasiwasi,  watarajie kupata vitu vizuri na tofauti zaidi... watapata  vitu vinono kwa vile tamasha hili linazidi kuwa bora zaidi.
 "Sikukuu ya Pasaka ni upatanisho kutokana na kifo cha Yesu Kristo aliyefia msalabani na kufufuka siku ya tatu... tutaienzi sikukuu hiyo kwa nderemo," alisema Upendo.
 Mwanamuziki huyo anayeabudu katika Kanisa la BCIC lililoko Mbezi Beach, Dar es Salaam (Kwa Askofu Gamanywa), alisema amejiandaa vyema kukonga nyoyo za mashabiki wake na mbali na
 kufanya mazoezi, pia atafunga na kusali ili Mungu amfanyie miujiza.
 Aliwaomba mashabiki wamiminike kwa wingi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Aprili 8 na Jamhuri Aprili 9, kuona mambo  mazuri aliyowaandalia na kuongeza kuwa kwa vile anamtukuza
 Mungu aliyemtoa kwenye shida na majaribu mengi ya Shetani, anaamini atawapa kile wanachotaka kutoka kwakwe.
 Alisema anatarajia kuimba nyimbo mbalimbali zikiwemo zilizotamba za Zindonga (alioimba kwa Kizulu), Unajibu Maombi na Ni Salama Rohoni. Kilahiro hivi sasa anatamba na albamu yake mpya ya Ficho Langu aliyoirekodi nchini Canada.

No comments:

Post a Comment